Kesi hiyo namba 107 ya 2010, ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Hawa Ngh’umbi dhidi ya Mnyika ambaye ni mdaiwa wa pili katika kesi hiyo akitetewa na Wakili Edson Mbogoro.

Mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo iliyoko mbele ya Jaji Upendo Msuya ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi (RO) katika jimbo hilo, (aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni) ambao walikuwa wakitetewa na Wakili Mkuu wa Serikali (PSA), Justice Mulokozi.

Katika uchaguzi huo, uliofanyika Oktoba 31, 2010, Msimamizi wa Uchaguzi, Raphael Ndunguru alimtangaza Mnyika kuwa mshindi Novemba 2, 2010 baada ya kupata kura 66,742. Ngh’umbi alipata kura 50,544.

Hata hivyo, Ngh’umbi hakuridhishwa na matokeo hayo akaamua kufungua kesi Mahakama Kuu kuyapinga, akimtumia Wakili Issa Maige.

Katika hati yake ya madai na wakati akitoa ushahidi  mahakamani, Ngh’umbi na mashahidi wake walidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu na kisheria katika ujumlishaji wa kura na utangazaji wa matokeo ambao umeathiri matokeo hayo.

Hoja za kuzingatia
Katika hukumu ya leo, Jaji Msuya atazingatia hoja tano ambazo zinatokana na madai katika hati ya Ngh’umbi alizozitoa wakati akitoa ushahidi wake mahakamani pamoja na mashahidi wake wawili, kuhusu ukiukwaji huo wa sheria.

Hoja hizo zitakazozingatiwa katika hukumu ya Jaji Msuya ni pamoja na kama mkanganyiko wa takwimu za kura katika Fomu namba 24B (Fomu za matokeo ya jumla ya ubunge), zimeathiri matokeo hayo ya uchaguzi mzima.

Hoja nyingine ni kama mlalamikiwa wa pili (Mnyika), aliingia na kompyuta (laptop) tano katika chumba cha majumuisho ya kura na kama ndizo zilizotumiwa na wasimamizi wa uchaguzi kuhesabu na kujumlishia kura.

Nyingine ni kama marekebisho ya kura katika baadhi ya fomu namba 21B, (Fomu za matokeo ya kura za ubunge vituoni), yalifanyika katika chumba cha majumuisho na mlalamikiwa Mnyika kuingia na kundi la wafuasi wake katika chuma cha majumuisho kinyume cha sheria.

Hoja nyingine ni kama mlalamikiwa wa pili (Mnyika) alitoa kauli za kashfa dhidi ya mlalamikaji (Ngh’umbi) kwa kumuita fisadi, akimtuhumu kuuza jengo la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT).
Wakati akitoa ushahidi wake mahakamani, Ngh’umbi alidai kuwa matokeo hayo siyo sahihi kwa sababu pamoja na mambo mengine, katika fomu ya matokeo yaliyotangazwa kuna kura 14,854, zisizojulikana mahali zilikotoka ambazo upande wa mashtaka unadai ni kura hewa.

Alisema kwa mujibu wa fomu hiyo, kura halisi zilikuwa ni 119,823, kura halali zilikuwa ni 117,639 huku kura zilizokataliwa (zilizoharibika) zikiwa ni 2,184.
Lakini alidai kuwa ukijumlisha kura zake na za Mnyika wote kwa pamoja kisha zikitolewa kutoka katika kura halali zilizopigwa, zinabaki kura 353 ambazo ndizo zitagawanywa kwa wagombea wengine 14, jambo ambalo alisema si sahihi.

Hata hivyo, wakati akijitetea, Mnyika alikanusha madai hayo yote licha ya kukiri kuwepo kwa mkanganyiko wa usahihi na uwiano wa kura katika Fomu namba 24B.
Lakini, bado alidai kuwa dosari hiyo zinaweza kurekebishwa na kwamba haziathiri matokeo kiasi cha kuyafanya yawe batili.
Shahidi wa kwanza upande wa wadaiwa (DW1), aliyekuwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Gaudence Kadiarara alikiri kuwa Mnyika aliingiza kompyuta hizo japo alidai kuwa hata hivyo, hawakuzitumia, tofauti na Mnyika ambaye alidai hakuingia na kompyuta yoyote.

Shahidi huyo na mashahidi wengine wa utetezi akiwemo Msimamizi wa Uchaguzi (Mkurugenzi wa Manispaa), pia walikiri kuwepo kwa mkanganyiko katika fomu ya matokeo hayo ya ubunge lakini, wakasisitiza kuwa dosari hizo haziathiri matokeo jumla.

Hoja hizo ndizo ambazo ama zitamshawishi Jaji Msuya katika hukumu yake kutengua matokeo ya ubunge huo au kuthibitisha kwamba matokeo hayo ni halali.

Mawakili wa utetezi, PSA Mulokozi kwa niaba ya AG na RO na Mbogoro kwa niaba ya Mnyika, walidai kuwa mlalamikaji ameshindwa kuthibitisha madai yake na hivyo kuiomba mahakama iyatupilie mbali.

Lakini, Wakili Maige anayemtetea Ngh’umbi alisema wamethibitisha madai yao kwa kiwango kinachohitajika kisheria na kuiomba Mahakama itengue matokeo hayo yaliyompa ushindi Mnyika.

Alisema madai mengine yameungwa mkono na mashahidi wa utetezi hususan DW1 aliyekiri Mnyika kuingia na kompyuta katika chumba cha majumuisho ingawa alikanusha kuzitumia tofauti na Mnyika aliyekana kuingiza kompyuta hizo katika chuma hicho.
Pia Wakili Maige alihoji sababu ya mawakili wa Serikali kutowaita mahakamani baadhi ya mashahidi ambao walitajwa na upande wa madai na wa wadaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika mchakato wa uchaguzi huo.

Wakili Maige aliwataja mashahidi hao ambao alidai walikuwa ni muhimu kuitwa mahakamani kujibu madai na kutoa ufafanuzi wa masuala yaliyowagusa kuwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mtaalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Mkurugenzi huyo alidaiwa kuwa ndiye aliyekagua kompyuta zilizotumika kufanyia majumuisho ya kura ambazo zilidaiwa kuwa zilitoka Manispaa ya Kinondoni, baada ya mfumo wa awali ulioandaliwa na Nec kuonekana kuwa haufai.

Lakini, Wakili Maige alidai kuwa kitendo cha kushindwa kumuita mkurugenzi huyo wa Nec mahakamani kutoa maelezo ya ukaguzi alioufanya na mbinu alizozitumia kuithibitishia mahakama kuwa katika kompyuta hizo zisingewezekana kuingizwa taarifa za kughushi ni kinyume cha sheria.

Akirejea kesi ya Stanbic Bank (T) Ltd dhidi ya Woods (T) Ltd namba 48 ya mwaka 2002, alidai kuwa Mahakama ilishatoa mwongozo kuwa ushahidi wa kitaalamu hauwezi kuthibitishwa kwa maneno matupu mpaka mtaalamu huyo atakapoitwa kuutolea ufafanuzi.

Wakili Maige alidai kuwa upande wa madai umethibitisha kuwa kompyuta zisizostahili kisheria ndizo zilizotumika kufanya majumuisho na kwamba ndizo zilizosababisha kuwepo kwa mkanganyiko uliojitokeza katika fomu ya matokeo wa kura zaidi 14,000, zisizo na maelezo.

Advertisements