Elizabeth Michael ‘Lulu’.

Na Wilbert Molandi
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela, hivi karibuni alizuiwa kumuona msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ aliye mahabusu kwenye Gereza la Segerea, Dar es Salaam.
Lulu amewekwa mahabusu kutokana na tuhuma za mauaji ya msanii maarufu wa filamu nchini, Steven Kanumba aliyefariki dunia zaidi ya siku 40 zilizopita nyumbani kwake Sinza, Vatican jijini Dar.
Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita majira ya saa nane mchana wakati katibu huyo alipofika gerezani hapo akiwa na familia yake kwa ajili ya kumjulia hali Lulu.
Akizungumza na na chanzo cha habari hizi, Mwakalebela alisema walipofika gerezani hapo, walitakiwa kutoa kibali maalum na walipotaka kujua sehemu ya kwenda kukipata, wahusika walidai wao hawafahamu.
Mwakalebela alisema walitumia zaidi ya dakika 45 kubembeleza ili waweze kumuona msanii huyo lakini waligonga mwamba.
“Leo (Jumapili) nimesikitishwa sana, nilifika Segerea na familia yangu, cha ajabu walikataa eti mpaka niwe na kibali maalum, jitihada zetu za kupata kibali ziligonga mwamba kwa madai kuwa twende ngazi za juu.
“Tuliomba watuelekeze huko juu ni wapi lakini cha ajabu nao walisema hawapajui kwani huwa wanaletewa majina tu, kwa kweli imetusikitisha. Tulichukua dakika 45 kuomba kuingia lakini ikashindikana, ikabidi turudi nyumbani,” alisema Mwakalebela.

Advertisements