MSANII chipukizi wa kundi la Tanzania House of Talent (THT), Winfrida Josephat ‘Rachel’ amewataka wasanii wenzake wa muziki wa kizazi kipya kuacha kuwategemea wakongwe wanapotaka kutoka.

Rachel, mmoja wa wasanii wanaochipukia katika kundi hilo, alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, msanii anayetaka kutoka, anapaswa kusimama mwenyewe.

Msanii huyo, ambaye kwa sasa anatamba na kibao chake cha Kizunguzungu, alisema msanii chipukizi anaweza kumshirikisha msanii mkongwe katika kurekodi nyimbo yake, lakini bado asiweze kutoka.

“Unatakiwa usimame wewe mwenyewe. Ningetaka kufanya hivyo, ningeweza kumshirikisha Barnaba au Linah, lakini nilitaka kutoka kivyangu,”alisema mwanadada huyo.

Rachel, ambaye anashabihiana kwa sura na umbo na msanii mkongwe wa fani hiyo, Rehema Chalamika ‘Ray C’ amesema, mafanikio aliyoyapata kimuziki katika kipindi kifupi yametokana na jitihada zake binafsi na pia kujiamini.

Alisema ili msanii aweze kupata mafanikio, anapaswa kufanyakazi zake kwa kujiamini yeye mwenyewe bila ya kutegemea msaada wa wasanii wakongwe.

Msanii  huyo ni mmoja wa wasanii wa kundi la THT hupata nafasi za kurekodi nyimbo zao baada ya kupita kwenye hatua mbalimbali.

Akitoa mfano, Rachel alisema baada ya msanii kutunga wimbo wake, anapaswa kuupeleka kwa viongozi wa kundi hilo, ambao huupitia mmoja mmoja kabla ya kutoa maoni.
“Wimbo wa msanii kabla ya kuamriwa urekodiwe, unapitiwa na watu wengi na kila mmoja atatoa maoni yake. Yupo atakayesema ufanyiwe marekebisho, mwingine atasema haufai, mwingine atasema kiongezwe kitu fulani, hivyo ndivyo utaratibu ulivyo,”alisema.
Image
Kwa mujibu wa Rachel, kwa sasa anajiandaa kurekodi nyimbo zake zingine kwa kushirikiana na kiongozi wa bendi ya Mashujaa, Charles Baba, Ray C na Barnaba.

Advertisements