Shakoor Jongo na Musa Mateja
Mwana-Bongo Fleva namba moja kwa sasa, Naseeb Abdul Jumaa ‘Diamond’ na staa wa filamu za Kibongo, Aunt Ezekiel Grayson wamenaswa laivu ndani ya Hoteli ya Grand Villa iliyopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam, chanzo cha habari kina mkanda kamili.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, Mei 16, mwaka huu, Diamond na Aunt walibambwa kwenye hoteli hiyo wakati mvua ikinyesha huku kukiwa na ‘kibaridi’, hali iliyosababisha watu kuamini kuwa huenda walikuwa na lengo la kuvunja amri ya sita.
Habari hizo zilidai kuwa Aunt ndiye aliyelipa fedha za chumba walipofika mapokezi kabla ya kuzama ndani.
Baada ya kuzinyaka habari hizo, mapaparazi wetu walimtafuta Diamond ili kupata undani wa sakata hilo ambapo alipopatikana, alikiri kutinga hotelini hapo.Katika maelezo yake, Diamond alisema anaomba kutumia nafasi hiyo kuweka mambo sawa kwani alishaanza kuchafuka mitandaoni hivyo alidai alifika mahali hapo kwa lengo la kukutana na jamaa yake kwa ajili ya mazungumzo ya kikazi.

“Ni kweli siku hiyo nilifika pale ila sikwenda kufanya chochote na Aunt.
“Ukweli ni kwamba pale kulikuwa na rafiki yangu wa karibu sana na huyo ndiye alikuwa na Aunt (mtu wa Aunt), mimi nilimsindikiza tu kwa sababu nilikuwa na mazungumzo kikazi na jamaa huyo,” alisema Diamond na kuongeza kuwa kama watu wanaohisi kuwa anatoka na Aunt wanakosea kwani anamchukulia kama shemeji yake. Kabla ya kumpata Aunt ili kupata undani wa ishu hiyo, alisikika akihojiwa Radio Clouds FM ambapo alikataa katakata kuwa siyo yeye bali alifananishwa.

Pamoja na kuelezwa stori nzima na kuambiwa kuwa kuna mtu aliwapiga picha wakiwa hotelini hapo, Aunt aliendelea kushikilia msimamo wake.
Ili kupata uhakika wa habari hizo, mapaparazi wetu walimtafuta Aunt. Alipopatikana alichanganya ulimi na kufunguka:

“Wale walionihoji mara ya kwanza waliniambia nimeonekana na Diamond nyuma ya Sayansi wakati mimi nilikutana na Diamond ndani ya Hoteli ya Kebby’s iliyopo Mwenge, sasa yawezekana waliyemuona ni mtu mwingine na siyo mimi.
Alipobanwa zaidi kuhusu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Diamond na walikutana ili kuvunja amri ya sita, Aunt aliendelea kuchanganya ulimi:
“Mimi na Diamond ni marafiki tu, tulikutana palepale, alipomaliza mazungumzo na mtu aliyemfuata kila mtu akachukua hamsini zake.”

Advertisements